IRENE ROBERT "SITALIA" NA CHRISTINA SHUSHO RASMI YOUTUBE

Mwimbaji anayefanya vizuri ndani na nje ya nchi ya Tanzania, Irene Robert, ameitambulisha rasmi nyimbo yake mpya "SITALIA". Nyimbo hiyo iliyo katika mfumo wa video tayari ipo katika platform mbalimbali ikiwemo youtube. Katika nyimbo hii muimbaji mashuhuri wa nyimbo za injili, Christina Shusho ameshirikishwa na kufanya muunganiko huu kutoa kitu bora kabisa mwanzoni mwa mwaka. Irene Robert ambae ni mshindi pia wa tuzo za MA.UP (Maranatha Africa Uprising Awards) zinazoandaliwa nchini Marekani, katika kipengele cha kolabo bora ya kimataifa aliyofanya na waimbaji Guardian Angel kutoka Kenya, Levixone kutoka nchini Uganda na Gaby Kamanzi kutoka Rwanda anaendelea kufanya vizuri siku hadi siku kutokana na ubora wa kazi anazozitoa.

"NIMESAMEHEWA" ya Paul Clement ndani ya HABARI MAALUM APP

Muimbaji wa nyimbo za Injili anayefanya vizuri nchini Tanzania, Afrika na hata nje ya Afrika Paul Clement ametoa wimbo wake "NIMESAMEHEWA" katika mfumo wa video ambao unapatikana rasmi ndani ya Habari Maalum App. Paul Clement alithibitisha hayo kupitia ukurasa wake wa Instagram, hivyo kama shabiki na mpenzi wa kazi na huduma ya Paul, unaalikwa kupakua App ya Habari Maalum ili uweze kuitazama.

HABARI MAALUM APP, KUINUA KIPATO WAIMBAJI NYIMBO ZA INJILI

Habari maalum kwa kushirikiana na BK Networks Co. Ltd wamewasilisha kwa jamii mtandao unaoweza kutumika kufanya mauzo ya kazi mbalimbali za Injili kwa njia ya kidijitali. Akiongea haya na Gospel Clinic, mkurugenzi wa BK Network Co. Ltd Eng. Kabenda Balete alieleza kuwa mfumo huu wa kidijitali umekuja kwa nia ya kuinua kipato cha waandaaji wa kazi za muziki, waandishi wa vitabu, watangazaji na waandaaji wa filamu. "Tumeona kuna changamoto kubwa katika mifumo mingine inayotumika kuuza kazi za wasanii na waimbaji, mifumo ambayo ni migumu na imekua ikiwakatisha tamaa walio wengi na kujikuta wakifanya kazi kwa gharama kubwa bila kurejesha sehemu ya gharama hizo kwa maandalizi ya kazi nyingine. Hii ndio sababu ya kuchukua jambo hili na kuliweka kama fursa kwa waimbaji na wadau wote wa Injili. Mfumo huu ni rahisi na salama, ambapo muweka maudhui anajiunga bure kabisa, na yule anaeingia kwa ajili ya kununua atahitajika kuwa na App hii pia na ataweza kununua kazi yoyote kwa kufanya malipo kupitia M-PESA, TIGO PESA, AIRTEL MONEY au VISA/MASTER CARD mfumo uliopo tayari ndani ya App. Karibuni wadau wote wa kazi ya Injili kusapoti kazi ya injili." alimaliza hivyo Eng. Kabenda.

CHRISTINA SHUSHO AANDIKA "THE ONE"

Mwimbaji wa kimataifa kutoka nchini Tanzania Christina Shusho, hivi karibuni kupitia ukurasa wake wa Instagram amekiweka wazi kitabu chake cha The One. Kitabu hicho ambacho amekinadi kuwa kitatoka hivi karibuni, Christina aliandika maneno ya kuwaomba wadau na wapenzi wa kazi zake na huduma yake kumpatia ushauri na yeye yupo tayari kuusikiliza. Christina Shusho ndie mwandishi wa kitabu hiki na tunamuombea kwa Mungu kiweze kutoka na kibariki maisha ya wengine.

J-SISTERS WAITAMBULISHA "NI WEWE"

Waimbaji wa nyimbo za injili kutoka familia moja J-Sisters, wameitambulisha rasmi video mpya ya wimbo wao uitwao ni wewe. Wimbo huo uliorekodiwa studio ya producer wa muziki wa injili Sam Yonah na video yake kufanywa na director Sesam pamoja na YK Media sasa upo kwenye platform mbalimbali za muziki ikiwemo youtube.

AMOS PROMOTION KUMLETA LUKALU

Waandaaji wa matamasha mbalimbali nchini, Amos Promotion wameamua kufungua mwaka kwa taarifa nzuri kwa wadau na wapenzi wa muziki wa Injili Tanzania. Kupitia kwenye mtandao wa kijamii wa Instagram, Amos Promotion wametambulisha tukio hili kubwa la kiinjili litakalo jumuisha waimbaji mbalimbali kutoka ndani na nje ya Tanzania, Debora Lukalu akiwa kama muimbaji mwalikwa kutoka nchi ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Waimbaji watakao kuwa wenyeji ni "Essense of Worship Team" wakati waimbaji wengine waliotambulishwa ni Paul Clement. Tunaamini list itakuwa kubwa na waimbaji wanaweza kuongezeka kulingana na ukubwa wa tukio lenyewe. Mega night of Celebration kama ilivyotambulishwa, itafanyika kanisani CCC Upanga tarehe 5 mwezi wa pili mwaka huu 2021 na hii ni kwa mujibu wa waandaji, huku viingilio vikiwa ni tsh 10,000 kawaida, tsh 20,000 VIP na tsh 30,000 VVIP. Ticket zinapatikana kwa njia ya malipo ya mtandaoni. Lipia kwa Tigo pesa 0659 700 001 AMOS WISTON MULUNGU kisha hifadhi namba za udhibitisho wa malipo, waweza kupiga simu namba 0745 500 522 kuhakiki malipo uliyofanya.

KIBONGE WA YESU AJA KIVINGINE

Muimbaji wa nyimbo za Injili maarufu kama Kibonge wa Yesu au Kibomelody aliyefanya vizuri katika nyimbo mbalimbali ikiwemo Hakuna, ametambulisha tena nyimbo yake mpya. Akiongea na Gospel Clinic, Kibo amesema wimbo huu aliouachia wenye mahadhi ya singeli sasa unapatika kwenye mitandao yote ya kijamii. "Wimbo huu video yake tayari imetoka na inapatika youtube pia" aliongezea Kibo. Ikumbukwe kuwa muimbaji huyu mwenyeji wa mkoani mbeya amewahi kufanya kolabo na waimbaji mbalimbali kama Ikupa Mwambenja, YZ Manamba na Rodgers Mathew, lakini katika wimbo huu mpya alioupatia jina la mbele kwa mbele amefanya kolabo na Imani Missana.

WALTER ASISITIZA "USINIPITE"

Muimbaji wa kimataifa wa nyimbo za injili nchini Tanzania, Walter Chilambo ametambulisha wimbo wake mpya "usinipite". Walter aliyefanya vizuri sana kupitia nyimbo zake mbalimbali ameuelezea wimbo huu kuwa ameuimba ili uwe sehemu ya ibada kwa mtu atakae usikiliza na apate kubarikiwa; "Wimbo huu ukawe ibada kwa kila mmoja katika yale tunayopitia na kumsihi Mungu asikupite juu ya yote, baraka zake na neema pia kibali katika kila jambo, ninawapenda sana na nina imani mtabarikiwa" aliandika hayo walter katika ukurasa wake wa Instagram. Wimbo wenye hisia na tungo mahiri unapatika kwenye mitandao ya kijamii pia Boomplay na youtube, utafute leo na ubarikiwe.

Previous post

THE PURPOSE AND POWER OF LOVE AND MARRIAGE

Next post

This is the most recent story.

Rodgers Mathew

Rodgers Mathew

Gospel Clinic Website Developer.

No Comment

Leave a Reply