“Hakuna madhihirisho pasipokuwa na maandalizi”
“There is no manifestation without preparation…”

Mit 16:1
Maandalio ya moyo ni ya mwanadamu; Bali jawabu la ulimi hutoka kwa Bwana.

         Siku zote neno la mwenye moyo safi hupokelewa na Mungu. Hivyo moyo ni eneo muhimu linalopaswa kuandaliwa kabla ya kwenda kukutana na Mungu. Kwa lugha rahisi, moyo ni madhabahu itumikayo kuweka sadaka iliyo safi mbele za Bwana.

Maandalizi makubwa ya moyo, huleta madhihirisho makubwa.

taz. (1fal 18:21-29) “…Kwa hiyo na watutolee ng’ombe wawili; wao na wajichagulie ng’ombe mmoja, wamkate-kate na kumweka juu ya kuni, wasitie moto chini; nami nitamtengeneza huyo ng’ombe wa pili, na kumweka juu ya kuni, wala sitatia moto chini. Nanyi ombeni kwa jina la mungu wenu, nami nitaomba kwa jina la BWANA; na Mungu yule ajibuye kwa moto, na awe ndiye Mungu. ….. wakamtwaa yule ng’ombe waliyepewa, wakamtengeneza, wakaliitia jina la Baali tangu asubuhi hata adhuhuri…. Lakini hapakuwa na sauti, wala aliyejibu, wala aliyeangalia.

         Mdahalo huu, baina ya Eliya na manabii wa Baali, ulikuwa unahitaji kuonyesha uwezo wa mungu ambaye angeonekana ana nguvu zaidi, yaani Mungu wa Eliya au mungu Baali. Hivyo maandalizi yalihitajika ili kufanikisha adhma zao.

Kwa upande wa manabii wa Baali walifanya maandalizi pia kwa kadiri ya taratibu walizoona zinawafaa Neno linatueleza “….wakamtwaa yule ng’ombe waliyepewa wakamtengeneza,…” Maandalizi yao yaliangalia zaidi ile sadaka iliyotolewa (ng’ombe) kuliko madhabahu.

Kwa upande wa Eliya, nabii wa Mungu aliye hai alijiandaa namna hii; taz (1waf 18:30-35) “…Kisha Eliya akawaambia watu wote, nikaribieni mimi. Watu wote wakamkaribia. Akaitengeneza madhabahu ya BWANA iliyovunjika. Eliya akatwaa mawe kumi na mawili, kwa hesabu ya kabila za wana wa Yakobo,…Naye akaijenga madhabahu kwa mawe hayo katika jina la BWANA; akafanya mfereji, kama wa vipimo viwili vya mbegu, ukiizunguka madhabahu. Kisha akazipanga zile kuni,akamkata yule ng’ombe vipande vipande, akaviweka juu ya kuni…

Eliya aliwaita watu wamkaribie yeye na watu “wote” walimkaribia, hii ikiwa kama ishara ya kujiamini na kuwa na imani kwa Mungu anayetaka kumdhihirisha. Baada ya hapo “akaitengeneza madhabahu ya BWANA iliyovunjika”. Kama nilivyokwisha kutangulia kusema moyo ulio safi hufanyika kuwa madhabahu ya Kristo, lakini moyo uliokata tamaa, moyo uliotumikishwa na adui ni ngumu kuwa imara mpaka uchukue hatua ya kujitakasa na kuanza na Bwana.

Maandalizi makubwa ya moyo huleta madhihirisho makubwa na ushindi. Eliya aliweza kumwabudu Mungu na kumtukuza mbele ya manabii wa Baali, baada ya kukamilisha madhabahu aliyokuwa akiiandaa. Taz (1waf 18:36-39)

Mungu hushuka na kupokea sadaka ya mioyo yetu, kama kuna maandalizi mazuri. Katika agano la kale, sadaka ilitolewa juu ya madhabahu iliyojengwa… na hata sasa sadaka iliyo njema ni ile itokayo katika moyo ulio safi.

Taz (mwa 22:9) “wakafika mahali pale alipoambiwa na Mungu, Ibrahimu akajenga madhabahu huko, akaziweka tayari kuni, kasha akamfunga Isaka mwanawe, akamweka juu ya madhabahu, juu ya zile kuni.

Ni maombi yangu leo mioyo yetu ifanyika kuwa madhabahu inayobeba maombi na sifa za Mungu, maana maombi na sifa ni sehemu ya dhabihu mbele za bwana.
Kitu kinachochipuka kutoka ndani ya moyo, huwa hakisahauliki na hakipotezi ladha yake. Huwa kina nguvu ya pekee.
Mara nyingi wanadamu tumekuwa tukitazama mwonekano wa nje, lakini Mungu hutazama ndani ya kilindi cha moyo wa mwanadamu.

Previous post

BEST OF SWAHILI GOSPEL (EAST AFRICA)

Next post

NAMNA YA KUFIKIA MALENGO

Rodgers Mathew

Rodgers Mathew

Gospel Clinic Website Developer.

No Comment

Leave a Reply