Wengi huwa na mipango na malengo mbalimbali bila kuangalia wamewekeza nguvu kiasi gani ya kuweza kutimiza malengo waliyonayo.”

Mawazo haya yanaweza kuwa rahisi tu, kama hauna mpango wa kuongozwa na Roho mtakatifu. Lakini kama wewe ni mmoja kati ya wale wajinyenyekezao mikononi mwa Bwana, ni swali la muhimu sana na la msingi kujiuliza.

        Kuna mambo mengi sana ambayo yamefundishwa na walimu mbalimbali kuhusiana na mambo haya ya malengo!, somo hili linaweza kukupatia baadhi tu, ila kwa uwezo wa Roho mtakatifu, atalihuisha ndani ya moyo wako na kukuzidishia maarifa zaidi.

 Mambo haya ndiyo tutakayo yatazama zaidi;

  • Malengo.  (Goals)
  • Matumizi ya Nguvu na Uwezo. (The useful of Ability and Power)
  • Mtandao. (Networking)
  • Matumizi ya muda. (Time using)

 MALENGO.

         Malengo ni mipango itarajiwayo kujidhihirisha ndani ya kipindi cha muda fulani. Ni ndoto iliyoandikwa mahali, ili iweze kutimia ndani ya muda fulani.

         Watu huwa na malengo tofauti tofauti kutokana na mipango tofauti. Watu waliofanikisha malengo au ndoto zao waliweza kufanya mambo haya mawili;

kwanza walipangilia malengo yao na pia walifuata hatua tofauti tofauti, ambazo waliona zinaweza kuwasaidia kufikia pale wanapo patazama. Kumbuka, kushindwa kupanga ni kupanga kushindwa. Watu wengi hushindwa kufanikisha malengo yao kwa sababu walishindwa ku-focus katika eneo lile analohitaji kufika. Tambua jambo hili, “concentration is the magic key that open the door to accomplishment”

Basi tunawezaje kupangilia malengo?

Kuna mahitaji makubwa matatu yanayohitajika kukusaidia.

  1. Orodhesha mambo yote unayohitaji kuyatimiza katika maisha yako, bila kuhusisha mambo ya jumla kama kuwa na furaha, kuwa tajiri nk. Badala yake weka vitu vya muhimu kwako mfano kupata shahada katika masomo yako au kupata kazi.
  2.  Orodhesha mambo yote unayohitaji kuyatimiza katika kipindi cha mwaka unaokuja. Mambo hayo ndiyo yatakayokusaidia kukupeleka katika malengo uliyoandika katika alama ya kwanza kama malengo ya kutimiza katika maisha.
  3. Orodhesha mambo yote unayohitaji kuyatimiza katika kipindi cha mwezi unaokuja. Mipango hiyo itakusaidia kufikia malengo yako uliyopanga kutimiza hapo baadae, baada ya mwaka au ndoto za maisha.

       Baada ya kupangilia orodha hiyo ndefu, hakikisha basi ni mambo ambayo ni ya msingi, na yanawezekana kufikiwa kama ukiimarisha nguvu na uwezo wako. Pia hakikisha ni vitu unavyo hitaji kweli katika maisha yako.

Mafanikio si kitu kinachokuja ndani ya siku moja tu, bali ni matokeo ya hatua ndogo ndogo na nidhamu ambayo itakuwa inasimamia kusudi ulilonalo moyoni.

         Unaweza ukatazama habari ya mtu mmoja aliyeitwa Habakuki nabii, aliyekuwa na shauku ya kuona mabadiliko katika taifa lake, ambalo kwa kipindi chake aliweza kuona udhalimu na kila aina ya ufisadi (Hab 1:1-4). Lakini kuna kitu cha kujifunza kutoka kwa nabii huyu wa Mungu, aliona kulalamika tu haikuwa suluhisho la kuweza kuona ndoto zake na mipango yake ikitimia katika taifa lile, yaani ndoto za kuona haki ikitendeka na amani kusitawi katika taifa. Hivyo alifanya hivi;

“Mimi nitasimama katika zamu yangu, nitajiweka juu ya mnara, nitaangalia ili nione atakaloniambia, na jinsi nitakavyojibu katika habari ya kulalamika kwangu.”(Hab 2:1)

Wakati mwingine mazingira yanayokuzunguka, mahali unapoishi,  panaweza kusababisha safari ya kutimiza malengo uliyonayo kuwa ngumu. Unaweza ukarejea tena Hab 1:1-4 utaona Habakuki aliishi katika maeneo yenye tabia ya namna gani. Lakini sura ya pili, Habakuki anatufundisha kuwa tunapoona njia tunayoitumia kuelekea kwenye malengo imezongwa na matatizo, tunahitaji kusimama katika nafasi zetu (maombi) na Mungu atatupatia maelekezo ni kitu gani tunatakiwa kufanya kwa wakati huo. Kwa upande wa Habakuki alijibiwa hivi;

“Bwana akanijibu, akasema, Iandike njozi ukaifanye iwe wazi sana katika vibao, ili aisomaye apate kuisoma kama maji. Maana njozi hii bado ni kwa wakati ulioamriwa, inafanya haraka ili kuufikilia mwisho wake; wala haitasema uongo; ijapokawia, ingojee, kwa kuwa haina budi kuja, haitakawia”

Una malengo au ndoto za namna gani? Bwana Yesu anatueleza wazi kuwa ni muhimu kuwa na mtazamo chanya katika kile tunachokisubiria. kuwa na nguvu ya kutosha kukomboa ndoto hiyo katika ulimwengu wa roho na uwezo wa kusubiri hata kipate kudhihirika katika ulimwengu wa mwili.

MATUMIZI YA NGUVU NA UWEZO.

          Nguvu na uwezo ni maneno ambayo yanategemeana kwa kiasi kikubwa. Nguvu ni uwezo wa kufanya kitu fulani, wakati Uwezo ni nguvu ya kuweza kufanya kitu fulani. Kwa mujibu wa kamusi ya kiingereza “Oxford Dictionary” wanatueleza; “Power is an ability of doing something” na “Ability is a power to do something”.

         Tunaweza kusimama vizuri katika yale tuliyoyapanga au tunayoyatarajia kama tuna uwezo na nguvu ya kutosha, sawasawa na malengo tuliyonayo. Nguvu na uwezo “power and ability” hutegemeana kwa kiwango kikubwa.

Unapoamua kupiga hatua na kutembea, mikono hufanya kazi ambayo watu wengi huona ni kazi ya kawaida tu, huenda mbele na kurudi nyuma kwa kupishana. Katika utaratibu huu miguu na mwili mzima hupata msawazo au “balance” nzuri na kuweza kusonga mbele kwa urahisi. Hivyo ndivyo ilivyo kwa nguvu na uwezo. Hii husaidia kuzaliwa kitu kipya kinachoitwa “potential”. Kwa sababu hii, ni wazi kuwa, tutaweza kufikia yale tunayohitaji kama tukiamua kupiga hatua na kuiachilia nguvu na uwezo uliopo ndani yetu uweze kufanya kazi.

Kwa maana imeandikwa;

(Taz. Efe 3:20)… “Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuyawazayo, kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu.”

Kuna mambo makuu mawili tunayoweza kujifunza katika mstari huo.

          Jambo la kwanza, “ Basi atukuzwe yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu mno kuliko yote tuyaombayo au tuwazayo…”

Mipango na malengo, mara nyingi imekuwa ikichukua nafasi kubwa kwenye maombi ya wapendwa wengi. Hivyo, huwa tunaamua kumshirikisha Yeye awezaye kufanya mambo ya ajabu.

Lakini atukuzwe kwanza, katika ukuu na uweza wa jina lake. “Jina lako litukuzwe…”

         Lakini jambo hili la pili, “Kwa kadiri ya nguvu itendayo kazi ndani yetu limekuwa mtego mkubwa kwa watu wengi. Wengi huwa na mipango na malengo mbalimbali bila kuangalia wamewekeza nguvu kiasi gani ya kuweza kutimiza malengo waliyonayo.

Pia tunahitaji kutambua kuwa, si kila nguvu inaweza kufanya kila kazi. “Nguvu kubwa huleta madhihirisho makubwa ila nguvu kidogo huleta madhihirisho kidogo”.

          Tunahitaji nguvu itakayoweza kutuwezesha kupata yale tunayohitaji kupata. Neno la Mungu linatueleza, ufalme wa Mungu hutekwa na wale walio na nguvu. Tukumbuke Bwana Yesu alipotufundisha kusali alisema;

“Basi msifanane na hao; maana Baba yenu anajua mnayohitaji kabla ninyi hamjamwomba. Basi ninyi salini hivi; Baba yetu uliye mbinguni, Jina lako litukuzweUfalme wako uje, Mapenzi yako yatimizwe hapa duniani kama mbinguni.Utupe leo riziki yetu.” (Mt 7:8-11)

         Mahali popote penye mamlaka ya kifalme, panahitaji nguvu. Utawala wowote usipokuwa na nguvu ni rahisi kuangushwa. Hivyo kama tulifundishwa kutojisumbua na mipango mingi tuliyonayo na maneno lukuki, tunahitaji sasa kulitukuza Jina la yeye awezaye mambo yote na kuomba ufalme wake ushuke. Kumbuka katika ufalme wa Mungu tunapata yote kwa sababu ni himaya ya Baba atupendaye, lakini tunahitaji nguvu ya ziada kwa maana ibilisi yupo akitunyemelea apate kutumaliza.

Hivyo tunawezaje basi kupata nguvu hizo? au nguvu hiyo itanisaidia nini katika malengo yangu ambayo ni ya kawaida na si ya kiroho? Haya ni maswali ambayo unaweza ukawa umejiuliza ndugu msomaji. Nguvu hii tunaipata kwa njia ya maombi. Tazama unapokuwa katika maombi ya muda mrefu kwa ajili ya hitaji fulani, nguvu ya kusonga mbele huingia ndani yetu, nguvu ya uwezesho huachiliwa juu yetu, hata kama tumechoka na kukata tamaa, Mungu ni mwema, kupitia maombi, malaika zake hushuka na kututia nguvu.

              Tunaweza kujifunza kitu katika safari ya Yesu ya kutimiza mpango wa Baba yake wa kuukomboa ulimwengu. Mpango huu ulihitaji kuwekeza maombi makubwa sana ili kuweza kuutimiliza. Achilia mbali maombi aliyoyafanya katika maisha yake ya nyuma, nahitaji tujifunze kitu katika maombi aliyoyafanya saa chache kabla ya kuingia kwenye mateso, pale katika mlima wa mizeituni. Taz (Lk 22:41-46)

           “Mwenyewe akajitenga nao kama kiasi cha kutupa jiwe; akapiga magoti akaomba, akisema, Ee Baba, ikiwa ni mapenzi yako, uniondolee kikombe hiki; walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.Malaika kutoka mbinguni akatokea akamtia nguvu. Naye kwa vile alivyokuwa katika dhikiakazidi sana kuomba; hari yake ikawa kama matone ya damu ya kudondoka nchi. Alipoondoka katika kuomba kwake, akawajia wanafunzi wake, akawakuta wamelala usingizi kwa huzuni. Akawaambia, Mbona mmelala usingizi? Ondokeni, mkaombe, msije mkaingia majaribuni.”

         Mpendwa, maombi haya hayakuwa maombi rahisi. Kama nilivyokwisha eleza awali kuwa, ibilisi anatuzengea apate kutuangusha. Hivyo, Bwana wetu Yesu kristo, alikuwa katika wakati mgumu wa kufanikisha kusudi au lengo la yeye kuwa hapa duniani, nalo si lingine, ni lile la kumkomboa mwanadamu. Hivyo katika hali hiyo ngumu aliyokuwa nayo ambayo imeelezewa kama dhiki, malaika kutoka mbinguni akatokea kumtia nguvu ya kusonga mbele naye akazidi sana kuomba!

“Walakini si mapenzi yangu, bali yako yatendeke.”Yesu alitamka.

Ndugu yangu, katika huduma yako au malengo uliyonayo, unakumbana na vikwazo gani? Je, ni kweli yote umeyakabidhi kwa Yesu ili afanye atakalo? Unaweza ukakata tamaa kutokana na unayoyasikiaunayoyaona au unayoyawaza, na hakika utaona hauna nguvu yakutosha kuendelea na mpango ulionao. Usikate tamaa, vaa utayari, uwe hodari na moyo wa ushujaa hilo tu! (Yos 1:18b).

Previous post

MAANDALIO YA MOYO

Next post

UFAHAMU NA MAARIFA

Rodgers Mathew

Rodgers Mathew

Gospel Clinic Website Developer.

No Comment

Leave a Reply